News Details

Ukatili Wa Viongozi Wa Kisiasa Katika Jamii.

Hivi karibuni kumekuwa na taarifa kuhusu aliyekuwa Naibu waziri wa Katiba na Sheria kutuhumiwa kunyanyasa mfanyakazi wake kijinsia,  #ChangeTanzania tunalaani tendo hili, Tukio hili la ukatili liliamsha mjadala mkubwa sana  katika mitandao ya kijamii hasa mtandao wa X kuhusu video iliyosambaa ya kijana H.A ( jina la kutunga kuficha utu wake)  akielezea ukatili aliofanyiwa na kundi la vijana wawili kwa maelekezo ya  aliyekuwa Naibu Waziri wa sheria na Mbunge wa Babati Pauline Gekul na waziri huyo ikielezwa alikuwepo wakati tukio lote linafanyika . Kijana  Anadai Gekul aliamuru Vijana hao wamuingizie chupa njia ya haja kubwa kijana H.A au wampige risasi kwa madai kuwa ametumwa kimkakati kwenda kwenye hotel inayomilikiwa na Gekul iitwayo Paleii Lake View Hotel. H.A  alikuwa ni mmoja wa wafanyakazi wa hotel hiyo. Baada kufanyiwa kitendo hicho cha udhalilishaji ndipo Pauline Gekul aliita polisi kuja kuwachukua yeye pamoja na mwenzake na kupelekwa kituoni ambapo walikaa siku nne bila dhamana na msaada wowote wa kiafya.

Pia kuna video nyingine ambayo inaonyesha Gekul akimhoji kijana H.A , video hiyo ikiaminika kuchukuliwa na Pauline, Video inaonekana H.A  akiwa uchi bila suruali na kumlazimisha akubali tuhuma zake kama ilivyoonekana katika video hiyo. Video hii inathibitisha kwa kiwango cha juu kwamba kulikuwa na tukio kati ya H.A na Gekul  lakini pia inafanana kwa kiwango kikubwa sana madai anayotoa H.A kufanyiwa na Gekul  Na pia usambazaji wa video hizo katika mitandao ya kijamii kulisaidia kueneza tukio hili la kikatili kwa haraka. Tunashukuru sana waliosambaza walizingatia utu wa kijana huyu kwa kuficha sura yake mwanzo wakati video zimeanza kutoka 

Wanasheria, wanaharakati, wanasiasa na Wananchi wa kawaida wapenda haki wamekemea na kulaani vikali tukio hili akiwemo Mwanaharakati Maria Sarungi nae amezitaka mamlaka kuchunguza tuhuma hizo na  kuchukua hatua stahiki juu ya sakata hilo. Alisema kupitia mtandao wa X Kijana huyu amedaiwa kulawitiwa na kuteswa na mbunge wa viti maalum mwanamke na naibu waziri! Polisi wanafunika na kijana huyo hana pa kugeukia isipokuwa mitandao ya kijamii

Tuhuma hizi nzito zinapaswa kuchunguzwa,  Rais Samia Suluhu - naibu waziri ndiye mteule wako! Ikiwa madai hayo ni ya uwongo ithibitike katika mahakama ya sheria” 

Jeshi la polisi limepokea mashtaka hayo na kutoa wito kwa mtuhumiwa kufika kituo cha polisi kwa mahojiano na yupo nje kwa dhamana. Jeshi la polisi   limesema kuwa linafanyia uchunguzi suala hilo. Wengi wamelalamikia utendaji kazi wa jeshi la polisi kuwa linafanya vipi uchunguzi huku mtuhumiwa akiwa hajakamwatwa, au kwa vile tuhuma za kosa hilo zimefanywa na kiongozi mkubwa katika nchi hii? Swali lingime wananchi wanajiuliza mbona viongozi wakikamatwa dhamana huwa ni haki ya kisheria ila ikija kwa wengine ni ngumu sana? Kama H.A  na mwenzake walikaa ndani bila kupewa dhamana kwa nini Pauline Gekul asingekaa ndani kipindi anachunguzwa kwa mashtaka hayo yanayomkabili?

Tatizo kubwa hapa ni mfumo mzima wa jeshi la polisi kuwa mbovu na sheria zetu hazina kipengele cha kuwawajibisha polisi endapo watavunja sheria ya kumkalisha zaidi ya masaa 24 mtuhumiwa ndio maana Hashim alikaa kwa takribani siku nne bila kuwepo kwa taratibu yoyote ile kisheria. Viongozi wote wa juu wa jeshi la polisi wapo lakini Gekul anapata wapi nguvu ya kufanya kitendo hicho bila kuogopa madhara yanayotokana na uvunjifu huo wa sheria na haki za Hashim Ally na mwenzake. 

Katika usambazaji ya video ya H.A , Bi  Paulina Slaa Narsis amehusika ili kupaza sauti ya H.A  isikike na kupata haki zake, ametoa taarifa za kutishiwa kuuwawa kwa kuchinjwa na kupigwa risasi na Emmanuel Gekul ambaye ni mdogo wa Pauline Gekul, lakini hadi sasa hakuna hatua yoyote imechukulia na jeshi la Polisi. Bila shaka RPC anajua vizuri hili suala. Emmanuel Gekul anasema jeshi la polisi Manyara kwake siyo lolote na haogopi. Je, ni kweli familia ya Gekul imelishika jeshi la polisi Manyara?

Hii inaashiria kuwa jeshi la polisi Manyara na Babati, wanakula njama za kutenda uhalifu kwa kushirikiana na familia ya GEKUL, wachukuliwe hatua za kinidhamu na kisheria. Hatutakiwi kuwa na watu katika utumishi wa jeshi la polisi wanaoshirikiana na wahalifu kutenda Uhalifu wa kutisha kwa binadamu wenzao.

Hatua ya kwanza ambayo imechukuliwa katika kumuwajibisha Pauline Gekul kwa tuhuma za ukatili na udhalilishaji ni uteuzi wake kutenguliwa na Rais Samia kutoka kuwa Naibu Waziri na kuwa kubaki kuwa mbunge. 

Safari hii chama cha Umoja Wa Wanawake Tanzania (UWT) kimetoa tamko na kukemea vikali tukio hili lililofanywa na mwanachama wao na kusema kinafanya uchunguzi juu ya tukio

Kumekuwa na historia ya viongozi kama Mawaziri Wakuu wa Wilaya na Mikoa na wengio kufanya ukatili kwa wananchi na kukaliwa kimya bila kuchukuliwa hatua yoyote au hatua ikichukuliwa wanaishia kushinda na kuendelea na maisha yao kama  kawaida.

Tunakumbuka tukio la aliyekwa Mkuu wa Mkoa Wa Dsm Paul Makonda alipovamia kituo cha kazi cha habari cha Clouds alibaki huru hata hatua zilipojaribu kuchukuliwa ilishindikana na hakuwajibika kwa Tukio hilo

Mfumo wa kuwajibisha viongozi umekuwa mgumu sana kutekelezeka pale ambapo mkuu wa nchi hii hajapenda au kuruhusu taasisi husika kama jeshi la polisi na mahakama kufanya uwajibishaji, hivyo suala la uwajishaji kwa viongozi wakubwa linabaki kuwa la kumpendeza Rais na si wananchi. Hata katika sakata hili la Mbunge Pauline Gekul Rais ana uwezo wa kutotengua katika nafasi yake Na kuviomba vyombo vya uchunguzi kufanya kazi yake, lakini hii haikufanyika hivyo, Pauline bado ni mbunge na mwanachama wa chama cha mapinduzi, na sasa kuna habari kutoka Babati kwamba Pauline Nasra aliyesaidia sana kutoa taarifa za ili tukio anashikiliwa na polisi eti kwa tuhuma za kuomba Rushwa kwa Gekul ili kuzima ili tukio, Pauline Nasra amepitia vitisho vikali wakati wote, lakini yeye ndiye anayeshughulikiwa na jeshi la polisi na sio Gekul anayeripotiwa kufanya tukio, Tunajua tuhuma za rushwa zinataratibu zake, kuna namna ya kuhakikisha TAKUKURU inapata ushahidi, lakini tukio hili eti Polisi wamepewa tu shutuma na Gekul na kumkamata Pauline Nasra na kumuweka ndani
Miongoni mwa matukio mengine aliyofanya Gekul ni kukataa kufanya mahojiano na mwandishi wa habari wa Gadi TV, akimtaka aende ofisini kwake, alipofika ofisi kwa Gekul alikamatwa kwa tuhuma kwamba Naibu huyo wa Waziri wakati huo alikuwa na mashaka na maisha yake, na mwandishi alikamatwa kwa kufika hapo  ofisini, wakati mwandishi huyo alikuwa anakwenda kuchukua taarifa ya upande wa Gekul kuhusu tukio ilo, kwa maana nyingine Gekul alikuwa anakwepa kuongea na vyombo vya habari na polisi wakamsadia kukwepa wajibu huo.

Tukio hili linatumbusha wananchi kuwa vita ya kutafuta #KatibaMpya lazima iendelee kwa kasi ili kurekebisha mifumo yote ya haki jinai pia kupunguza madaraka ya Rais ambaye hufanya uwajibishaji atakavyo na si kwa maoni ya wananchi au hata udhibiti wa sheria ndogo ndogo za maadili zilizopo nchini.

#ChangeTanzania

0 Comment

Leave a Comment