Walionipiga risasi wako wapi? Amepatanisha nini wakati maridhiano yana giza kali - Lissu.
Mara ya mwisho nilipokuja kufanya mkutano ilikuwa ni mwezi Julai mwaka 2011 tena nilikuja na katibu wetu Dk Slaa , ile siku tuliyofanya mkutano hapa kijana anayeitwa Ally Zona aliuawa kwa kupigwa risasi na polisi wakati wakituzuia tusifanye mkutano hapa (miaka 12 imepita tangu siku hiyo). Nilipokuja kipindi kile hawakuwa wananiita Chiba ila leo wananiita Chiba kwa sababu ya mambo mabaya yaliyofanyika katika nchi hii, Kuna watu wengi waliouawa toka tumefanya mkutano tangu Ally Zona alipouawa hapa ni wengi hawana idadi. Wengine wamepotea wamechukuliwa katika famila zao na nyumba zao hatujui walipo hadi leo.
Nchi imejaa mabango kila mahali kuwa ameunganisha nchi, ameondoa uhasama swali;
Je hawa waliouwawa wameuwawa na nani?
Waliomteka Ben Saananae mpaka leo hatujui alipo ni akina nani?
Tumeunganishwaje wakati hatuambiwi watu waliouwawa wameuawa na akina nani waliomuua yule mwanafunzi Akwilina siku ile viongozi wetu wamekamatwa, alipigwa risasi mchana kweupe, je hao ndugu zake wamepatanishwa lini?
Je mjane wa Alphonce Mawazo aliyekatwa mapanga saa tisa za mchana amepatanishwa lini?
Watu zaidi ya 400 wameuwa Kibiti, Rufiji na Kuna mtu alikuwa na kiwanda cha madawa hapa Dar Es Salaam amekamatwa kiwandani kwake mchana kweupe na hajaonekana mpaka leo. Na walionifanya mimi leo naitwa Chiba ni akina nani na mimi nimepatanishwa lini?
Sasa haya mabango ni ya nini? Nimeona nimewekwa kwenye mabango Dar Es Salaam nani aliyewaambiwa mniweke mimi kwenye mabango kwamba nimepatanishwa? Mwenyekiti wetu Freeman Mbowe alikuwa Gaidi mwaka jana tu eti leo amepatanishwa, sasa kuna upatanisho au kuna kusanifiana tu? Tunapatanishwa au tunapangwa tu ili tukubali kufunika makombe maharamia yapite? Hakuna dhambi mbaya katika nchi iliyopitishwa kama tulikopitishwa sisi, tusidanganyane.
Askari polisi waliostaafu 2020 hawajalipwa stahiki zao za kustaafu na nauli za kurudi makwao mpaka leo. Na sio polisi tu ni kila mfanyakazi wa nchi hii.
Kuna mahali panaitwa Kiegea hapa Morogoro wananchi wananyang’anya ardhi zao na mkuu wa mkoa anaongoza polisi kwenda kunyang’anya watu mashamba yao. Maelfu ya watu kule Mbarali Mbeya wananyang’anywa mashamba yao vijiji karibu 20 na zaidi, wanapelekewa jeshi na nyumba zinachomwa moto, ukihofu unawekwa ndani na polisi. Wananchi wanaumizwa na serikali yao ukiuliza kwa nini badala upewe majibu wanakazana kupamba mabango ya upatanishi nchi nzima. Watu wanatekwa na hivi karibuni nimepewa taarifa kuwa watu wanaoishi Dar Es Salaam kule Mabwepande upande wa Wazo wanaambiwa waondoke lile eneo ni la DDC (Dar Es Salaam Development Cooperation) wakati ilianzishwa mwaka 1971 na kufungwa mwaka 1974, sasa hivi watu wanapelekewa Jeshi na Amos Makala ( mkuu wa mkoa wa Dar Es Salaam) kuwa wahame. Tukija Ngorongoro peke yake takwimu zinasema watu elfu na ishirini waondolewe kwa nguvu wapelekwe mahali panaitwa Msomera, Handeni Tanga . Serikali ilipewa pesa shilingi bilioni 35 ya kuhamishwa Maasai kuwapeleka Msomera na ikaliwa, waliokula pesa wanajulikana ila ukihoji unaambiwa nani kama mama.
Mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu nchini Tanzania katika ripoti yake mwaka huu ukijumlisha wizi na uchafu wote uliofanyika tunapata jumla ya zaidi ya Trilini mbili za kitanzania. Ukipita msamvu hapo kuna bango la TRA lina picha ya mama linasema lipeni kodi ili tujenge nchi pamoja, sasa najiuliza nilipe kodi ili tujenge nchi au nilipe kodi ili walaji wale? Hii nchi inaupigaji mkubwa, wanaposema kazi iendelee wanataka kazi ipi iendelee? Maana ufisadi wa mwaka huu ni mkubwa kuliko ufisadi wa mwaka jana na ufisadi wa mwaka jana ni mkubwa kuliko ufisadi wa mwaka juzi. Kila mwaka ufisadi unazidi na unafanywa na watu wale wale ambao wanatuambia kazi iendelee. Sasa kampeni ya uchaguzi wa mwaka 2025 zimeanza na zimeanza kwa katiba hii hii tuliyonayo ina maana hawataki kubadilisha katiba.
Sisi tunataka #KatibaMpya ili twende katika uchaguzi ujao tukiwa na #KatibaMpya , Tume mpya huru ya uchaguzi , sheria mpya za uchaguzi na majimbo mapya ya uchaguzi. Mfumo wetu wa uchaguzi ni uchafu mtupu ambao lengo lake ni kuhakikisha CCM inabaki madarakani Tumepeleka mapendekezo ya maridhiano na tumenza mazungumzo toka mwaka jana mwezi Mei , sasa ni Mwaka umepita , Lakini mapendekezo tuliyopeleka kitu gani kifanyike? Na tumeweka wazi kabisa kwamba nini kifanyike na nani afanye nini? Na kifanyike vipi ili tupate #KatibaMpya , lakini Tangu tunepeleka mapendekezo hatujajibiwa hata moja mwaka ujao ni uchaguzi wa serikali za mitaa na vijiji , unafikiri tutakwenda kugombea kwa sheria ipi kama sio ile enguaengua ya mwaka 2009? Na tukienda kwa sheria hiyo tutegemee nini? Mpaka sasa hakuna mwenye matokeo ya urais ya Magufuli na Samia Hasssan 2020 hayapo , hivyo hakuna Rais aliyechaguliwa ni ametangazwa tu kwa sababu kura zinatakiwa kuwepo katika gazeti la serikali lakini mpaka leo hakuna, Na katika uchaguzi ule wa 2020 Morogoro ndio iliyoongoza kwa wabunge waliopita bila kupingwa. Kuna jimbo linaitwa Misungwi lina kata 27 tuliweka mbunge na madiwani kataka kata hizo lakini wote walienguliwa na CCM ikapita bila kupingwa. Hivyo ninaPozungumzia suala la kupata katiba mpya ni ili haya yasijirudie.
Matatizo yote tunayopitia mfano suala la uporaji wa ardhi, maisha magumu, kuporomoka kwa viwanda ni kwa sababu ya walioko madarakani na chama chao. Viongozi waliopo madarakani wanapenda sana kumsema Magufuli kwa sababu amekufa , lakini ukweli ni kwamba wote ni washiriki wa hii dhambi ( matatizo yanayoendelea kuwapa wananchi nchini) dhidi ya watanzania
Kwa mujibu wa katiba ya sasa na sheria zote za nchi hii Rais wa sasa ni MUNGU mtu kwa sababu Rais akiamua jambo lolote hata liwe baya linatekelezwa. Mfano akimua wananchi wachukuliwe fedha zao zilizotengwa na Bunge zinachukuliwa na zimechukuliwa. Ripoti ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa Serikali kabla haijapelekwa bungeni anakabidhiwa Rais kwanza halafu ndio anaagiza ipelekwe bungeni hivyo anayejua wizi uliogunduliwa na mdhibiti na mkaguzi mkuu wa serikali ni Rais , je mpaka leo amechukua hatua yoyote? Jibu ni Hapana na marais wote waliopita hawajawahi kuchukua hatua yoyote katika hili , hivyo ninapozungumza katiba mpya nataka mtu mmoja asipewe nguvu ya kufanya maamuzi ambayo yanaweza kutuumiza kama ambavyo tunaumizwa . Tunataka tupate katiba ambayo kama tunamtaka mkuu wa mkoa au wa wilaya tuwachague wenyewe na wakishindwa kutekeleza majukumu tuwaondoe wenyewe. Kama kweli kuna maridhiano mchakato wa katiba mpya uko wapi? Utaratibu wa kupata katiba mpya mwaka ujao kama tulivyopendekeza uko wapi?
Tuwe na kauli moja kuwa tusipokuwa na katiba mpya kabla ya uchaguzi ujao hapatakalika, tusidanganyane.
Ujumbe wangu ni kuwa tudai katiba mpya na mfumo mpya wa uchaguzi, mfumo mpya wa Haki zetu kabla ya uchaguzi mkuu ujao. Tukienda katika uchaguzi mkuu ujao kwa katiba hii hii iliyopo yatatokea ya 2019 na ya 2020, anayetuambia kuwa wamebadilika kwani Magufuli aliyafanya yote peke yake ? aliosaidiana nao ni akina nani na wako wapi? Hivyo tusikubali maneno ya upatanisho wakati hakuna chochote unachokiandaa kutupatia katiba mpya”. — Tundu Lissu
#KatibaMpya #ChangeTanzania
0 Comment
Leave a Comment