Miaka Miwili Bila Magufuli, Miaka Miwili na Samia 20 MARCH 2023.
Imetimia miaka miwili tangu kifo cha Rais wa Awamu ya Tano John Pombe Magufuli. Kuna mengi sana yanazungumzwa na Watanzania wengi wanakumbuka awamu ya tano kutokana na mfumo wake wa utawala au namna walivyoendesha nchi, awamu ya tano ilitambulika kama awamu ya maamuzi bila kujali sheria au kwa kutunga sheria mpya ili kuzifuata hizo sheria ambazo nyingi zililalamikiwa na watu, awamu ya tano kwa kifupi ni aina ya utawala ambao ulikuwa na mikakati ya kuwa na sheria ambazo walizijenga kwa misingi ya kujipambanua kama utawala wa sheria, lakini sheria nynigi zilikuwa na utawala mkubwa na ziliumiza watu,
Awamu ya Tano ilitunga sheria nyingi kwa wakati mmoja baada ya kupata changamoto kutoka kwa wadau mbalimbali kwa kusema ulikuwa utawala wa kidikteta, ili kujinasua na hali hiyo walitumia mbinu ya kutunga sheria zinazoendana na kila wanachotaka kufanya, sheria nyingi lizikuwa zinalenga watu, taasisi au mfumo au biashara au kundi la watu, malengo ya kuwa na hizo sheria ni kama tulivyoeleza ilikuwa ni kujenga utawala wa sheria yaani utawala unaofuata sheria lakini sheria za namna gani basi ni hizo walizotengeneza wao kwa malengo maalumu.
Moja ya sheria iliyobadilisha ilikuwa ni sheria ya kampuni na NGOs na hapa walikuwa wakilenga NGOs na mashirika binafsi ambayo yalikuwa akifanya kazi ya uraghbishi, sheria ilizuia makampuni yaliyokuwa yakifanya uraghbishi nchini na kuyalazimsha yote kuwa NGOs, na sheria ya NGOs ilibadilishwa ili kumpa msajili wa NGOs nguvu kubwa ikiwemo kufuta NGOs kwa kadri anavyotaka bila nguvu ya mahakama, tukumbuke kwamba sheria ya makampuni walau inaruhusu makampuni kwenda mahakamani kama yataonewa au usajili wake utafutwa, makampuni yana haki ya kwenda mahakama ya biashara, lakini kwa NGOs kwa sasa hali ni tofauti zinaweza kufutwa tu pale msajili anavyotaka na hakuna nafasi ya kwenda mahakamani. Lengo kubwa hapa ilikuwa ni kujenga mazingira ya serikali kuwa na nguvu kufanya chochote kwenye hizi NGOs.
Sheria nyingi iliyotungwa ilikuwa ni sheria ya uhujumu uchumi na pia kukiri makosa ya jinai, lakini sheria hii ilijengwa kwenye mazingira magumu kwa watuhumiwa, mfumo wake ilikuwa inalenga kupora haki za watu kunyanyasa watuhumiwa, malengo makubwa ikiwa ni kuipa nguvu serikali kudhibiti wafanyabishara, wanasheria na wanaharakati mbalimbali nchini.
Sheria nyingine mbaya ni ile ya vyombo vya habari na sheria ya masuala ya uharifu wa kimtandao, malengo makubwa yakiwa ni kukwamisha ukosoaji na pia kuondoa habari za uchunguzi, sheria zote mbili ziliondoa kwa kiasi kikubwa sana haki ya wananchi kupata habari na kuruhusu upande mmoja wa serikali kutoa taarifa ambazo zilikosa kitu kinachoitwa check and balance, kila ilichosema serikali ndicho kilikuwa ukweli, hakuna habari za uchunguzi ambazo ziliruhusiwa sababu magazeti mengi sana yalifunngiwa kwa wakati huo. Hii ilitoa nafasi kubwa sana kwa serikali kupotosha kwa masuala mengi na kupotosha kuhusu miradi mingi na hakuna namna zaidi ya wananchi kupata habari za upande mmoja tu.
Moja kubwa ambalo utawala wa awamu ya Tano ulifanya ilikuwa ni pamoja na kudhibiti mikutano ya vyombo vya habari, suala hili ilikuwa ni kuondosha kabisa hali ya uhuru wa watu kukusanyika, mikutano mingine yote iliathirika pia, baada ya zuio hili mikutano mingine kama ile ya AZAKI kuelimisha wananchi nayo ilidhibitiwa kimya kimya, japo ile ya vyama vya siasa ilikuwa ni agizo la waziwazi,
Serikali pia ilitunga sheria ya TAKWIMU, sheria hii ni moja ya sheria mbaya sana kuwahi kutoka nchini, sheria hii ilimpa nguvu MTAKWIMU kumiliki takwimu zote, hakuna mtu aliyeruhusiwa kufanya tafiti bila kibali chake, hakuna takwimu zinaruhusiwa nchini bila kupewa kibali, na kibali hiki ni kuanzia wakati wa kufanya utafiti na wakati wa kutoa takwimu zenyewe, kwa maana nyingine mtakwimu ndiye anayeendesha kila kitu kunzia utafiti wenyewe na mpaka kutoa takwimu yenyewe, hii inaondoa uhuru wa watu kufanya tafiti bila kuingiliwa na serikali, hakuna uhuru wa kutengeneza taarifa bila serikali kuweka mikono hivyo kudhibiti mambo yote ambayo serikali haivipendi. Sheria hii imetumika sana kusaidia serikali kuwa na taarifa za kiuchumi na maendeleo bila mbadala wa vyombo huru pia kufanya tafiti na namna hiyo bila kuingiliwa na serikali.
Serikali ya awamu ya tano pia ilithibiti watoto wa kike kupata haki ya elimu, kupitia maagizo ya Rais Magufuli kulipigwa marufuku kwa watoto wa kike kurudi shule baada ya kujifungua , ndipo kampeni ya #ArudiShule ilipoanza na ile ya #ElimuBilaUbaguzi kampeni zote mbili zilikuwa na madhila kwa walioshiriki kuzifanya zikiwemo NGOs, kuna NGOs zilifungiwa kwa kushiriki kampeni hizi lakini pia pamoja na hayo imekuwa kampeni endelevu kudai haki ya watoto wa kike kupata elimu hata wakati huo mgumu wa Rais Magufuli
Haya ni baadhi ya mambo ambayo yaliyoyafanywa katika utawala wake yake ikiwemo Marufuku za Rais Magufuli ambazo ziliathiri wananchi, uhuru na Haki zao:
- Kupingwa Mafuruku Matangazo mubashara ya bunge;
Mwanzoni mwa 2016, serikali ya Magufuli iliminya matangazo hayo kwa kuanza na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) na baadae mpaka kwa televisheni binafsi. Matangazo mubashara ni yale ya kipindi cha maswali na majibu tu. Mijadala haiKkurushwi mubashara tena. Nape Nnauye, ambaye alikuwa waziri wa habari wakati huo, aliitetea uamuzi huo akisema kuwa ilikuwa ni mzigo mzito kifedha kwa TBC kurusha matangazo hayo mbashara. Alisema kwa siku moja TBC ilikuwa ikiingia gharama ya Tsh 4.2 sawa na dola milioni 1.8. Pia alidai kuwa Tanzania si nchi ya kwanza katika Jumuiya ya Madola kufanya hivyo.
Lakini Rais Magufuli alikuwa akizunguka na TBC nchi nzima na kila mahali anapokwenda bila vikwazo vyovyote vya gharama kwa shirika ili
- Wanafunzi wanaopata ujauzito;
Serikali ya MagufulI iliendeleza katazo la wanafunzi wanaopata ujauzito kuendelea na masomo baada ya kujifungua. Hata hivyo, Magufuli amezuia jitihada za kuondosha katazo hilo ambalo limedumu kwa muda mrefu hadi sasa. https://drive.google.com/file/d/1QgZgR9nedV3DKQW0V38HFMzbbNQvbxh4/view?usp=share_link
- Mikutano ya siasa
Mara baada tu ya kuingia Ikulu, Magufuli aliweka wazi msimamo wake kuwa hatopenda kuwaona wanasiasa wakizunguka nchi nzima kufanya mikutano ya hadhara. Kuanzia hapo mikutano ya hadhara na majukwa ya siasa kwa ujumla yalizuiliwa kwa wapinzani na kupelekea Chama kikuu cha upinzani cha Chadema kutangaza operesheni ya kupinga kile walichokiita Udikteta Tanzania (UKUTA) na kudhamiria kufanya maandamano ya nchi nzima mwaka 2016, lakini waliisitisha kabla ya kuanza. Toka kipindi hiko, polisi waliwashughulikia viongozi wa upinzani wanaodaiwa kukaidi marufuku hiyo - na takriban wabunge 17 wa upinzani walifikishwa mahakamani kukabiliana na mashtaka.
- Aliminya uhuru wa habari na kujieleza kwa ujumla wake.
Kwa kutunga sheria kandamizi dhidi ya uhuru wa habari, pia vyombo vya habari kadhaa vilifungiwa kwa muda tofauti kwa kutangaza ama kuchapisha taarifa ambazo mamlaka inadai kuwa ni 'chonganishi' ama zenye 'kupotosha' umma. Lakini pia mwaka 2017 aliwaonya wamiliki wa vyombo vya habari kuwa wajiangalie, na kuwa hawana uhuru kwa kiasi wanachofikiria.
- Kutekwa, kupotezwa, kuumizwa na kubambikiwa kesi kwa wanasiasa na wanaharakati - Wasiojulikana kufanya kazi bila wasiwasi
Baada ya kuingia madarakani Magufuli alitengeneza mkakati kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kuwaumiza wananchi wote ambao walikua wakikosoa ama kwenda kinyume na utawala wake. Wanaharakati mfano, Tito Magoti na Theodory Giyani, walifikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashtaka matatu ya uhujumu uchumi. Mwandishi wa masuala ya uchunguzi nchini Tanzania Eric Kabendera aliwekwa mahabusu kwa zaidi ya miezi sita kwa kesi ya kukwepa kodi, Azory Gwanda, Ben Saanane na wengineo. Serikali ya Rais Magufuli haikufanya juhudi zozote kuondoa wasijulikana, wala kufanya operation ya kutafuta wasiojulikana , Lakini tuliona akiibuka mtu aliyetambulika kama Mwanaharakati Huru Musiba akitisha watu na kutukana watu, akapewa mpaka fursa ya kutengeneza gazeti ambalo lilikuwa na wadhamini likiwemo SHIRIKA la Ndege ATCL ambalo likuwa na matangazo kwenye gazeti hili, Gazeti ambalo lilikuwa linaendika uzushi na kuchafua watu, lakini pia watu wote walioumizwa hakuna aliyelipwa fidia au kusakwa kwa watu waliowaliohusika
- Kupigwa Risasi ,
Moja ya tukio baya sana kuwahi kutoka nchini katika siasa ni kupigwa risasi kwa mwanasiasa Tundu Lissu, lakin serikali ikakataa kumpa huduma ya matibabu, bunge likaondoa haki zake zote za malipo na matibabu, lakini serikali ikasema haihusiki na shambulio hilo, japo matendo yake yalileta maswali mengi, imekuje basi ikagoma kumtibia? Imekuwaje basi ikamuondolea haki zake za malipo kama mbunge wakati ambao akahitaji sana fedha kwa kujitibia na kujikimu ?
- Katiba Mpya ;
katika utawala wa Magufuli aliweka wazi kutoendelea na mchakato wa katiba mpya ambao ulinzishwa na Rais wa nyuma yake Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Magufuli alikataa kabisa michakato ya kuboresha sheria nchini , hakutaka nchi kupata msiingi bora ya utawala.
- Miaka miwili ya Mama Samia madarakani:
Samia Suluhu Hassan ndiye mwanamke wa kwanza kuwa Rais nchini Tanzania. Samia aliapishwa siku ya Ijumaa tahere 19/03/2021 katika ikulu ya jijini Dar es Salaam. Kwa mujibu wa katiba ya Tanzania, Rais Samia Suluhu Hassan atahudumu kwa kipindi kilichosalia cha muhula wa Urais wa Awamu ya Tano, Japo kuna watu wanasema hii ni Awamu ya Sita kitu ambacho kinazua sana mjadala mpaka, kwa sababu katiba inasema wazi makamu atamaliza kipindi kilichobaki na sio kipindi kipya cha awamu, lakini ili tutalicha kuwa mjadala wa siku nyingine,
Baada ya kifo cha Rais John Pombe Magufuli na Rais Samia kuingia Madarakani alianza kwa mambo yote ya Magufuli na kusema yeye ni sawa na Magufuli, alichukua sheria zote zote za Magufuli ambazo zinaendelea mpaka leo, alichukua miradi yote ya Magufuli na wateule wote wa Magufuli pia aliendelea nao, Rais Samia hajawahi kuteua waziri Mkuu kama Katiba inavyotaka, na kisha yeye na waziri Mkuu kushauriana kuunda baraza la mawaziri hii hajafanya pia, kwa maana nyingine kuna ukakasi kikatiba kwa namna alivyounda baraza la mawaziri kwa sababu waziri mkuu wa sasa Kasimu Majaliwa hana kiapo kwa Rais Aliyepo madarakani, aliapa kwa katiba na kutia Rais Magufuli sio Samia. Hili tatizo lipo mpaka leo na ni tatizo la kikatiba.
Katika kipindi cha awamu ya 5 Rais Samia alikuwa ameshika wadhifa wa makamu wa Rais, kipindi ambacho kilikuwa na ukiukwaji wa haki na demokrasia, haki za binadamu na kutungwa sheria ngumu na mbaya sana kuwahi kutokea nchini, ukiukwaji ulikuwa ni kwa kiwango kikubwa sana, watu waliporwa mali zao na wengine waliumizwa vibaya sana na vyombo vya dola na mamlaka ya mapato TRA.
Mara baada ya kuingia madarakani, Rais Samia alianza kujipambanua kama yeye ni Magufuli yeye na Magufuli ni sawa, baada ya changamoto za uchumi kuzidi na msukumo wa umma, tuliona kidogo kidogo alionyesha kwa umma ahadi ya kutafuta uwanja wenye usawa kidemokrasia, alianza na msema wa 4R, kisha akaunda KIKOSI KAZI, kikosi kazi ilikuwa ni moja ya mbingu chakavu ambayo ilipingwa sana na umma, mwanzo alisema watamsaidia kuboresha masuala ya kidemokrasia na ushauri kuhusu sheria zinazokwamisha demokrasia nchini, kwa bahati mbaya sana aliunda kikosi kazi na kuweka watu ambao kwa asilimia kubwa walikuwa ni dhaifu na pia walioshangilia uchaguzi 2020 Mfano Mkandara kupitia Redit walisema uchaguzi ulikuwa huru na wa haki, Baadaye alikutana na vyama vya siasa hasa CHADEMA ambao waligoma kushiriki katika kikosi kazi, kwa malengo ya kutaka kujenga demokrasia, umoja na amani na kuweka mazingira sawa ya kisiasa. Kuna matokeo kwenye hili vyama vya siasa kwa sasa vinaweza kufanya mikutano yao ya kisiasa, Hii ikiwa ni moja ya agizo la Rais Samia alipoingia madakarani akijaribu kutumia mbinu za Magufuli, lakini alishindwa na kuruhusu mikutnao ya vyama vya siasa kufanyika
Katika kipindi cha miaka miwili ya Rais Samia kuna masuala ambayo bado anayapa kisogo ambayo hayaonyeshi nia ya dhati ya kulikomboa Taifa hili. Nayo ni kama yafuatayo
- #KatibaMpya : katika awamu zote za utawala wa CCM katika nchi hii suala la katiba mpya limekuwa likipigwa danadana na kusogezwa mbele na wakati mwingine mchakato kuanzishwa na kuishia njiani kwa kuwa ni dhahiri kuwa katiba hii ni dhaifu na ina mapungufu mengi na kupelekea kila serikali inapoingia madarakani kuwa na utawala wa kibabe kwa nguvu kubwa ambayo anakuwanayo Rais. Katika hotuba yake ya hivi karibuni ambayo aliitoa katika mkutano wa wanawake BAWACHA, alipokuwa mgeni rasmi Rais alisema kuwa suala la mabadiliko ya katiba ni la mageuzi na ni la taratibu huku akiahidi kuuanza kulifanyia kazi bila kutaja wakati mchakato huo utakapoanzia. https://www.youtube.com/live/2cxJTxMxclo?feature=share HAKUNA sababu za msingi mpaka sasa kwa nini mchakato wa #KatibaMpya umeshikiliwa na serikali ya Rais Samia wakati huo huo akisema yeye anapigania demokrasia
- Uhuru wa Mahakama; uhuru wa mahakama bado unaonekana kuingiliwa kwa maslahi serikali na chama cha mapinduzi, kwa kiasi kikubwa sana serikali inajisafisha sana kupita mahakama, mfano mzuri ni Kesi ya Ugaidi ya Mbowe na Kesi nyingi za mashekhe, serikali ikitaka kufanya suala baya kwa mtu kutumia mahakama na ikitaka kukandamiza mtu pia tumeona mahakama inatumika, kuna Watanzania wengi wako mahabusu kwa miaka mingi kwa sababu serikali inataka iwe hivyo, na siku serikali ikiondoa nia ya kesi hizo kesi zinafutwa, hakuna siku mahakama imetoa maagizo kufuta kesi zenye mwelekeo usio na ushahidi wa kutosha ambazo zinajulikana kama tunaendelea na UPELELEZI, HALI HII BADO INAENDELEA hata wakati huu wa Rais Samia akiwa madarakani, lakini hivi karibuni aliyekuwa mbunge wa Arusha mjini Godbless Lema wakati anataka kurudi Rais Samia alisema kwamba alimwambia aje na akamfutia kesi, haya ni maneno ya Rais mwenyewe kwamba kwa mazingira yaliyopo ni yeye anayeweza kutaka kesi iendelee au iondolewe, Kwa kauli ya Rais alimuahidi kuzifuta na hatimae akarejea nchini, hii ni katika hali ya kutaka kuonyesha kuwa sasa maridhiano ya kisiasa yanaendelea vizuri, lakini hii sio sawa katika misingi ya utawala bora kwa sababu hakuna Mtanzania anayetakiwa kuwa na kesi sababu Rais ametaka hivyo au kufutiwa kesi kwa sababu pia Rais amependa hivyo, lakini kwa upande mwingine katika siku ya wanawake alipoulizwa kuhusu hatma ya wabunge wanawake 19 alijibu kuwa suala lipo mahakamani na hawezi kuingilia mahakama, hivyo bado kuna mkanganyiko wa uhuru wa mahakama nchini. https://www.youtube.com/live/2cxJTxMxclo?feature=share na bahati mbaya zaidi suala la Wabunge 19 sio la kimahakama ni suala la Spika kutaka wabunge hao mahakamani, hakuna kesi mahakamani inayozuia wabunge hao kuondolewa, wabunge hao wanakesi mahakamani dhidi ya chama chao wakitaka kurudishiwa uanachama, lakini kwa sasa hawana unanachama wowote hivyo kupoteza sifa ya kuwa wabunge.
- Wanafunzi wanaopata ujauzito; Tangu Rais Samia aingie madarakani wanafunzi wanaopata ujauzito HAWAJAPATA nafuu yeyote, Rais wa sasa kuwa Mzanzibar ambapo huko watoto wanarudishwa shule baada ya ujauzito na kuwa mwanamke hili suala lilionekana kuwa jepesi sana kwake, lakini kumekuwa na propaganda kubwa sana kuhusu suala hili ila ukweli ni kwamba watoto wake hawana haki ya kuendelea na masomo baada ya kujifunga, hakuna mfumo wa kuondoa na kurudisha watoto hawa shulenu kama ilivyo kwa Zanzibar, inawezekana vipi Rais anayetoka upande moja wa Muungano ambao una utararibu mzuri kurudisha watoto shule (http://idc-tz.org/news/the-spinsters-and-single-parent-children-protection-act-2005) ameshindwa kufanya hivyo kama suala la Muungano? Mpaka sasa hakuna mswaada wowote bungeni kuhusu utararibu na sheria ya kuwarudisha shuleni wanafunzi wa kike waliopata ujauzito baada ya kujifungua .
- Uhuru wa habari na kujieleza; katika kipindi cha miaka miwili ya Samia alipongia tu madarakani alifungua magazeti japo kwa masharti ya kwenda kuzungumza na waziri, hakuna uwazi wa nini kilichozungumzwa huko, lakini pia tumeshuhudia mikasa ya vyombo kupigwa faini na vingine kunyimwa leseni, Vyombo vya habari vilivyokuwa vimefungiwa katika kipindi cha awamu ya tano ilitumika sheria ambayo mpaka sasa bado iko na serikali ya Samia haijafanya juhudu yoyote kuondosha sheria mbaya za vyombo vya habari na ile ya matumizi ya mitandao au makosa ya mtandao ,
Changamoto ya pili kwa vyombo vya habari ni agizo la Waziri wa Habari Nape, kwamba vyombo vya habari viwe makini katika kutoa habari za mikutano hiyo, na ikiwezekana wasirushe mubashara wafanye record na kisha kuhariri na kurusha, hii ni ishara ya kukosa uhuru wa habari kwa sababu tishio hili la waziri linawanyima wanahabari haki ya kutoa habari kama zilivyotokea lakini kuzihariri kama anavyopenda waziri. Hii imefanyika wakati huu wa Serikali ya Rais Samia, alichomaanisha waziri wa habari Nape Nnauye alivionya vyombo vya habari kuchuja maudhui na wasilete habari kama zilivyo. Kauli hiyo haikukoselewa na Rais hiyo ikionyesha kukubaliana na hicho kilichosemwa na waziri huyo. Pia gazeti la Demokrasia february 27, 2023 lilizuiwa kusambazwa kwa siku hiyo likiwa tayari limeshachapwa kufuatia tukio hili bado uongozi wa Samia una changamoto katika suala zima la uhuru wa habari na kuzuia habari ambazo wanahisi wao zitawaharibia utawala wao.https://drive.google.com/file/d/1rTlzswaajRwbzQEkPd_qZvcojgsggqnb/view?usp=share_link. Kuna muendelezo wa matukio ambayo yamekuwa yakiashiria kuwa katika utawala wa Samia hadi sasa bado wananchi wanaokosoa serikali wanawekewa vikwazo mtangazaji Gerald Hando alikosoa suala la Rais kukopa sana pesa nje na ilipelekea kupoteza ajira yake lakini alikuwa ana haki kikatiba ya kutoa maoni juu ya suala hilo.https://drive.google.com/file/d/1fE0lT-aU8ZyL5dC9t5aHWaJoGj3No5_l/view?usp=share_link - Suala la utekaji na wasiojulikana; katika kipindi cha miaka miwili ya Samia inaonekana bado kuna muendelezo wa matukio ya kutekwa kwa watu na tuhuma muda mwingine zikienda kwa polisi na watu hao kutoonekana tena kama vile tukio la vijana watano waliotekwa Kigamboni, https://twitter.com/mariastsehai/status/1495637621393043460?lang=en na kijana Williaam sije ambaye alichukuliwa na polisi na kutoonekana tena na Baba yake mzazi alipita ngazi zote kutaka kujua mtoto wake yuko wapi lakini hakuna kilichoendelea. https://drive.google.com/file/d/1Fuvfb_kP-eg1fsBeD2xhMsK76wSVoTMU/view?usp=share_link. Pia matishio kwa wanasiasa wa upinzani walioonekana kukosoa serikali yameendelea kama ilivyotokea kwa kijana Nicholaus clinton wa NSSR Mageuzi alipotekwa na wasiojulikana na baadaye kupatikana akiwa na hali mbaya na hakuweza kuzungumza chochote. https://twitter.com/MariaSTsehai/status/1620379360325931010
Hii inafanya tuone kuwa utawala wa Samia bado una mapungufu yale ambayo yapo katika awamu zote zilizoongoza Chama Cha Mapinduzi.
- Kutobadili sheria kandamizi zilizopitishwa awamu ya tano; katika kipindi cha awamu ya tano kulipitishwa sheria ambazo ziliongeza kinga kwa watu ambao hawatakiwi kushtakiwa, hii inashusha uwajibikaji na kuongeza kasi ya watumishi na viongozi kutokuwa waadilifu wakijua fika kuwa hawawezi kuwajibishwa popote pale. sheria ya Mtandao ambayo ilitumika zaidi kuuzima uhuru wa kujieleza kwa wananchi. Katika kipindi hiki cha Samia hakuna sheria iliyobadilishwa na zote zinaendelea kutumika kukandamiza Watanzania. Kuna sheria nyingi kandamizi zilizotungwa wakati wa Magufuli lakini mpaka leo sheria zote hizo bado ziko na zinaendelea kutumika.
- Tume Ya Haki na Maridhiano ya Kitaifa; Wakati wa Rais Magufuli watu wengi waliumizwa , watu kutoka jamii zote walipata changamoto kuna wanaharakati, wafanyabiashara pia wanasiasa, kwa bahati mbaya sana serikali ya Rais Samia imeshindwa kabisa kuponya Taifa na makundi yote yaliyoathirika, tunaona kuna juhudi ya kuweka sawa mambo ya wanasiasa lakini kuna ukimya na giza kubwa sana kwa makundi mengine yaliyoumizwa na awamu ya tano, Je hii ina maana gani? Kwa nini Rais anashindwa kuondoa vikwazo kwa watu waliowekewa redflag kwenye passport zao, Mfano Prof Wajakoya aliyekuwa Wakili wa Lema na Watanzania wengine wengi waliokuwa wanatafutwa na serikali ya Rais Magufuli kutokana na kutofautiana na serikali yake.
- Mauaji Ndani ya jeshi la Polisi; Kuna malalamiko mengi sana kutoka kwa wananchi kuhusu mauaji ya polisi, Mwaka Jana tuliona video kutoka Serengeti Polisi wamefanya mauaji ya mzee mwenye familia, ambaye ni ndugu wa aliyekuwa Mbunge Catherine Ruge, Baadaye aliibuka Mzee William Sije naye akilalamika kuhusu mwanae kupotezwa na Jeshi la Polisi , amefuatilia sana bila mafanikio, lakini haya yamefanyika wakati wa serikali ya Rais Samia
- Kuporwa Ardhi Maasai wa Loliondo; Chini ya Rais Samia tumeshuhudia ukatili mkubwa sana kwa wakazi wa Ngorongoro hasa Loliondo, Wananchi wameporwa ardhi yao kinguvu, nguvu kubwa ya dola imetumika na kusababisha watu kukimbia nchi na wengine kusadikiwa kupoteza maisha wakikimbia maporini, sheria ya ardhi haikuheshimiwa kabisa na serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, masuala ya wananchi kuporwa ardhi yameenea sana mpaka huko Mbarali katika mabonde ambayo wananchi wamekuwa wakilima mpunga na kulisha nchi kwa miaka mingi.
Mwisho na kwa umuhimu sana ni miaka miwili ya Rais Samia bila mchakato wa katiba mpya , hakuna dalili njema mpaka sasa kuelekea kupata #KatibaMpya Kwa mambo hayo kadhaa yanayoendelea nchini ili Rais Samia aonekane ana nia thabiti ya kulikomboa Taifa hili jambo la kwanza la muhimu kuliko yote analotakiwa kufanya ni kubadili katiba hii ya sasa na kuleta katiba itakayoleta haki, uhuru na usawa kwa wananchi wote na kuondoa changamoto zote ambazo zinaonekana zipo kwa ajili ya uwepo wa sheria mbovu nchini.
#WenyeNchiWananchi #ChangeTanzania #KatibaMpya
0 Comment
Leave a Comment