Taarifa Ya Mdhibiti Na Mkaguzi Mkuu Wa Hesabu Za Serikali Kuhusu Ukaguzi Wa Miradi Ya Maendeleo Kwa Mwaka Ulioishia Tarehe 30 Juni, 2018.
Taarifa hii imelenga kuwapatia wadau wetu uchambuzi wa hoja mbalimbali zitokanazo na jumla ya kaguzi 469 za miradi ya maendeleo 87 ambazo Ofisi yangu ilikagua kwa mwaka ulioishia tarehe 30 Juni 2018. Miradi hii kiujumla inafadhiliwa kwa fedha za Serikali ya Tanzania pamoja na Wadau wa Maendeleo.
Nimezipanga hoja za ukaguzi katika makundi matatu, ambayo ni udhibiti wa usimamizi wa kifedha, utendaji wa miradi, pamoja na usimamizi wa manunuzi na utawala.
Kwa mwaka wa fedha 2017/18, kwa ujumla, miradi hii ilikuwa na kiasi cha shilingi trilioni 2.65 ambapo katika fedha hizo, kiasi kilichotumika ni jumla ya shilingi trilioni 1.64 na kubakiwa na bakaa ya shilingi trilioni 1.01 hadi kufikia tarehe 30 Juni 2018.
Kulikuwa na mapendekezo 5,686 kwa ajili ya utekelezaji kwenye miradi ya maendeleo kwa mwaka wa fedha unaoishia tarehe 30 Juni 2018. Kati ya hayo, mapendekezo 1,991 sawa na asilimia 35 yalitekelezwa; mapendekezo 1,000 sawa na asilimia 18 yanaendelea kutekelezwa; mapendekezo 1,953 sawa na asilimia 34 hayakutekelezwa; na mapendekezo 742 sawa na asilimia 13 yamepitwa na wakati. Katika mwaka wa fedha 2017/18, nimetoa hati zinazoridhisha 455 na hati zisizoridhisha 14.