Ripoti Ya Mwaka Ya Mdhibiti Na Mkaguzi Mkuu Wa Hesabu Za Serikali Kuhusu Ukaguzi Wa Mashirika Ya Umma Kwa Mwaka Wa Fedha 2017/2018
Ofisi yangu imeendelea kutekeleza majukumu yake vizuri kwa kufanya ukaguzi katika maeneo ambayo yasipoangaliwa vizuri yanaweza kuathiri ustawi wa nchi. Ripoti hii imekusanya masuala muhimu yaliyojitokeza katika kaguzi za Mashirika ya Umma kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018. Pia, imejumuisha mapendekezo yaliyotolewa kwa wasimamizi wa mashirika hayo ili kupunguza mapungufu yaliyojitokeza wakati wa ukaguzi. Hata hivyo, maelezo zaidi yamo katika ripoti husika za Mashirika.
Ripoti hii ina jumla ya sura 19 ambazo zimekusanya mambo muhimu yaliyojitokeza katika kaguzi za Mashirika ya Umma na Taasisi Nyingine za Umma ukiwemo mwenendo wa hali ya kifedha, uwezo wa kuendelea kutoa huduma, usimamizi wa mapato na matumizi, utawala bora na ufanisi katika utendaji wa Mashirika.
Kutokana na Serikali ya awamu ya tano kusisitiza umuhimu wa ujenzi wa uchumi wa viwanda kote nchini, nilipitia uwekezaji uliofanywa na Mashirika ya Umma ili kuangalia mapungufu, chanzo cha matatizo pamoja na kutoa mapendekezo ili kutatua mapungufu yaliyopo. Pia, kutokana na mwenendo mbaya wa Benki zinazomilikiwa na Serikali, ripoti hii imejumuisha mwenendo wa Benki hizo na kuonesha maeneo ambayo yanahitaji kuboreshwa.
Pamoja na kupongeza juhudi za Serikali katika kuunganisha Mifuko ya Jamii kwa lengo la kupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza ufanisi katika utoaji huduma, pia nimetoa mapendekezo katika maeneo ambayo yanapaswa kuboreshwa ili malengo hayo yafanikiwe.
Pia, ripoti hii imejumuisha ukaguzi katika Mamlaka za Maji ili kuangalia mwenendo wake katika kusimamia jukumu la upatikanaji wa maji, hatimaye kusaidia maendeleo ya nchi. Pia, imejumuisha ukaguzi wa manunuzi na usimamizi wa mikataba katika Mashirika ya Umma kwa kuwa ni sehemu ambayo pesa nyingi za Umma hutumika, pamoja na usimamizi wa Mali za serikali.
Nimeendelea kufanya kaguzi maalumu na kaguzi za kiuchunguzi (forensic audit) kwa Mashirika ya Umma, ambapo Muhtasari wa matokeo ya kaguzi hizo na mapendekezo yake nimeyajumuisha katika ripoti hii.
Ninayo matumaini kuwa mapendekezo ambayo nimeyotoa katika ripoti hii yatafanyiwa kazi na Mashirika husika. Pia, Serikali itafuatilia utekelezaji wa mapendekezo hayo