Report Details

Ripoti Kuu Ya Mwaka Ya Mdhibiti Na Mkaguzi Mkuu Wa Hesabu Za Serikali Juu Ya Ukaguzi Wa Taarifa Za Fedha Za Serikali Kuu Kwa Mwaka Ulioishia Tarehe 30 Juni, 2018

Ripoti hii inatoa muhtasari wa matokeo ya ukaguzi wangu wa taarifa za fedha za Serikali Kuu kwa mwaka wa fedha 2017/2018. Mawanda ya ukaguzi katika Serikali Kuu ni pamoja na Wizara na Idara za Serikali 65, Wakala 33, Mifuko maalum 16, taasisi nyingine 42, Vyama vya Siasa 14, Sekretariati za Mikoa 26, Balozi za Tanzania 41, Bodi za mabonde ya Maji 14. Pia, inajumuisha ukaguzi wa Mamlaka ya kodi ya mapato Tanzania (TRA), Hesabu Jumuifu za Taifa, ukaguzi wa awali wa mafaili ya mafao ya wastaafu na kaguzi maalum.

Hati za Ukaguzi

Lengo la kufanya ukaguzi wa taarifa za fedha ni kuwaaminisha watumiaji wa taarifa hizo kama zimeandaliwa kwa usahihi katika maeneo yote, na taarifa za fedha zina ujumbe unaohusu kipindi husika kwa kuzingatia miongozo ya utoaji taarifa na sheria zilizotumika. Taarifa ya ukaguzi huwapa watumiaji habari za uhakika kuhusu kiwango cha taarifa za fedha, kwamba ni sahihi na za kuaminika kwa kuzingatia taratibu zilizotumika na kubaini kuwa, hazina dosari. 

Matokeo ya ukaguzi yanaonesha kwamba, kati ya taarifa za fedha 241 zilizokaguliwa bila kujumuisha Vyama vya Siasa, 234 (97%) zilipata hati zinazoridhisha. Hawa ni wakaguliwa ambao taarifa za fedha hazikuwa na dosari yoyote; hii inamaanisha kuwa miamala ya fedha katika taarifa ni sahihi 7 (3%) zilipata hati yenye shaka; hapakuwa na hati isiyoridhisha wala hati mbaya.

Matokeo ya ukaguzi wa vyama vya siasa kwa taarifa za fedha za mwaka 2017/2018 yanaonesha kwamba, vyama vya siasa 14 vilikaguliwa 3 (21%) vilipata hati zinazoridhisha; 4 (29%) vilipata hati yenye shaka; 5(36%) vilipata hati mbaya; na 2 (14%) vilipata hati isiyoridhisha. Hii inamaanisha kuwa, taarifa za fedha za vyama vya siasa zilikuwa na dosari katika miamala ya fedha. Maelezo ya kina yanapatikana sura ya pili ya ripoti hii.


Posted on : 13 April, 2019 DOWNLOAD REPORT