TUNA SHERIA ZINAZO KINZANA NA HAKI ZA BINADAMU NA MAENDELEO .

Haki za Binadamu ni misingi, nyenzo ama nguzo ya maadili inayotakiwa kutumika kwa manufaa ya binadamu wote duniani na kwa usawa. Kifungu cha kwanza cha mkataba wa haki za binadamu wa mwaka 1948 umeainisha

“Watu wote wamezaliwa huru, hadhi na haki zao ni sawa. Wote wamejaliwa akili na dhamiri, hivyo yapasa watendeane kindugu”

Tanzania ina historia ya kipekee katika utekelezaji wa haki za binadamu toka tumepata uhuru mwaka 1961 Mpaka hivi sasa, Katiba ya kwanza ya uhuru ya mwaka 1961 haiku orodhesha haki za binadamu kwa mantiki hiyo hakukuwa na nia dhamiri kwenye ulinzi wa haki za binadamu.

Hata hivyo kulikuwa na sababu mbalimbali zilizokuwa zikitolewa na serikali zikiwemo, kwa kuwa tulikuwa tumetoka katika utawala wa kikoloni ilitupasa tujenge uchumi kwanza kisha baadae ndio tuimngize haki hizo katika katiba yetu.

Kutokuingizwa kwa haki za binadamu katika katiba ya mwaka 1961 serikali pia ilihofia mkanganyiko wa kisiasa ambao ungetokea baina ya mihimili ya serikali, yaani kati ya ule unaotengenza sheria (Bunge) na ule unao tafsiri sheria (Mahakama), kwani sheria mbazo zingekwenda kinyume na haki za binadamu zinge batilishwa.

Kucheleweshwa kuingizwa kwa haki za binadamu katika katiba pia kulichagizwa na kukosekana kwa upinzani wa kutosha wenye kuhamasisha serikali kuingiza haki hizo kwenye Katiba ya nchi.

Kuchelewesha kuingizwa kwa haki za binadamu katika katiba ya nchi ilipelekea kutengenezwa kwa sheria mbalimbali ambazo zilikuwa zinapoka haki za binadamu mfano, Preventive Detention Act, 1962 (No. 60 of 1962) na Deportation Act

Kuchelewesha kuingizwa kwa haki za binadamu pia kuli pelekea uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu hivyo kupelekea wananchi wengi kwenda kudai haki zao katika mahakama, Hata hivyo mahakama hazikuwa na msaada kwani utekelezaji haki za binadamu haukuwa umeainishwa na Katiba ya nchi bali zilikuwa zimetajwa tu katika utangulizi wa katiba.

Kutokana na kutokuingizwa haki za binadamu katika Katiba Uvunjifu wa haki za binadamu ulipitiliza ikapelekea wasomi mbalimbali, mashirika yasiyo ya kiserikali na wanaharakati kuanza kuhamasisha uingizwaji wa haki za binadamu katika katiba ya nchi, hata hivyo serikali ilipata shinikizo kubwa kutoka mataifa mbalimbali na msukumo uliokuja baada ya Tanzania kutia saini mkataba wa haki za binadamu wa mwaka 1948.

Katiba ya uhuru ya mwaka 1961 hai kuingiza haki za binadamu, Katiba ya jamhuri ya mwaka 1962 pia hai kuingiza haki hizo, vile vile katiba ya mpito ya muungano ya mwaka 1964 na ya mwaka 1965 zote hazikuingiza haki za binadamu na hatimaye ni marekebisho ya katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 yaliyofanyika mwaka 1984 ndiyo yaliingiza Haki za binadamu katika Katiba.

Sheria ya mabadiliko ya katiba ilitoa kipindi cha neema cha miaka mitatu kabla ya utekelezaji wa haki hizo, ilitegemewa katika kipindi hiki serikali ingekaa kuangalia kama kuna sheria yoyote inayokinzana na haki za binadamu zingerekebishwa na kuondolewa kabisa lakini haikua hivyo sheria ziliendelea kuwepo.

Licha ya Katiba ya mwaka 1977 kuweka haki za binadamu, toka zilipoanza kutekelezwa mwaka 1986 bado imeonekana kuna mapungufu makubwa katika haki hizo kama zilivyoainishwa katika Ibara ya 12 mpaka ya 32 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hili limedhihirishwa na kuwepo na sheria nyingi zinazokinzana na haki za binadamu pamoja na kuwepo na uvunjifu mkubwa wa haki hizo.

Moja ya pungufu kubwa lililopo katika haki za binadamu kama ilivyo ainishwa na Katiba ni kuto kuwepo kwa baadhi ya haki za msingi za binadamu, mfano Haki ya Elimu, Haki ya uraia, Haki ya mtuhumiwa na mfungwa, Haki za wafanyakazi na waajiri pamoja na Haki ya makundi maalum. Kuto Kuwepo kwa haki hizi kunacha giza kukosekana kwa utekelezaji wake.

Baadhi ya haki za binadamu zilizoainishwa katika katiba zimewekewa mipaka katika utekelezaji wake, mipaka hii inaondoa moja kwa moja uhalali wa mwananchi kufurahia haki kama zilivyoainishwa katika katiba, mfano Ibara ya 12-29 imeainisha  haki za binadamu, Lakini ibara ya 30 ya katiba hiyohiyo imeipa serikali nguvu ya kutunga sheria zinazopoka haki hizo.

Kuwekwa mipaka katika utekelezaji wa haki za binadamu unapelekea serikali kutunga sheria mbalimbali zinazikinzana na haki za binadamu, na mipaka hii inaondoa uhalali la katiba kuwa na nguvu kuliko sheria ndogo ndogo zinazotolewa na serikali kupitia bunge.

Siku za karibuni kume kuwa  na utengenezaji sheria mbalimbali zinazokinzana na haki za binadamu kwa mujibu wa katiba  na sheria hizo zimekuwa zikiendelea na uharamu wake kutokana na udhaifu uliopo katika katiba ya jamhuri wa muungano wa Tanzania 1977, Mfano Sheria ya Takwimu Na.9 ya Mwaka 2015 ambayo inazuia uhuru wa kujieleza kama ilivyo ainishwa katika ibara ya 18 ya katiba.

Hivyo basi kunahitajika mabadiliko makubwa ya katiba ili kuondoa changamoto na kurekebisha mapungufu yaliyopo katika haki za binadamu kama zilivyo ainishwa katika katiba ya jamhuri ya Tanzania.Leave a Reply