t

Update

TERMS AND CONDITIONS

Welcome to our website. If you continue to browse and use this website, you are agreeing to comply with and be bound by the following terms and conditions of use. If you disagree with any part of these terms and conditions, please do not use our website.

The use of this website is subject to the following terms of use:


You may not do any of the following while accessing or using the Change Tanzania platform and services:


Kwa Nini Tunajali....?

 

Imewasilishwa

Kamati ya Bunge ya Sheria na Mambo ya Katiba

Tarehe 22 Juni 2019

Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati hii

Tumepokea kwa heshima kubwa mwaliko wa kuchangia maoni kwenye zoezi muhimu la mapitio ya marekebisho madogo ya sheria mbalimbali kwa kuwasilisha uchambuzi wetu wa maandishi juu ya marekebisho yanayopendekezwa.

Tunaunga mkono juhudi za serikali zinazolenga kuleta uwazi zaidi, uwajibikaji na ushirikishwaji mpana kwenye kazi za mashirika mbalimbali ya kiraia, na pia dhana ya kuboresha tija na ufanisi zaidi kwenye kuratibu vyombo hivi.

Tunapongeza mabadiliko kadhaa muhimu yaliyoletwa kwenye kila sheria hizi. Wakati huo huo tunapendekeza maboresho katika maeneo kadhaa ili kuweza kutengeneza sheria ambazo zinakidhi mahitaji.

Marekebisho haya kwa pamoja yanaleta mabadiliko makubwa kwenye muundo mzima wa sekta ya AZAKI. Ni jambo la msingi sana kwetu sote kuhakikisha tunafikiri kwa pamoja na kwa makini kuhusu matokeo na madhara yanayoweza kutokea kutokana na marekebisho haya kabla ya kuharakisha kuyapitisha 

Ukusanyaji wa maoni toka wadau muhimu katika sekta hii unasaidia kuleta mawazo, uelewa na mitazamo tofauti kuhusu hoja zilizo mezani, pia yanasaidia kutafuta njia nyingi za kufanikisha jambo na kupata ufumbuzi bora. Ushiriki wa wadau mbalimbali unapelekea kupunguza matokeo hasi yasiyotarajiwa, kusaidia kuhamasisha wadau kwenye maamuzi na utekelezaji mzuri wa maamuzi hayo. Kwa hiyo, tunasisitiza kuwa kuwapatia wadau siku mbili tu kuchambua sheria na kujipanga kusafiri kuja Dodoma hakutoi muda wa kutosha kutafakari maswali haya muhimu.

Hivi karibuni tumeshuhudia maamuzi yaliyofanywa kwa nia njema lakini yakasababisha matokeo mabaya yasiyotarajiwa, kwa kuwa yaliharakishwa. Kwa mfano, Sheria ya Takwimu iliyorekebishwa, ilisababisha kusitishwa kwa Misaada ya maendeleo inayohusiana na takwimu, na sasa inarekebishwa tena ndani ya kipindi cha chini ya mwaka mmoja. Pia tuna mifano ya sheria zinazopitishwa, lakini zikapingwa mahakamani kwa kipindi kifupi tu tangu kupitishwa kwake, (mfano, Sheria ya Vyama vya Siasa ). Na mahakama zikaona kuna kesi zinazostahili kusikilizwa au hata kutoa ushindi kwa washitaki kufuatia kupitishwa kwa haraka kwa sheria mpya, mfano hukumu zilizopitishwa katika Mahakama ya Afrika Mashariki kuhusu Sheria ya Vyama vya Siasa, na Sheria ya Huduma za Vyombo vya habari. 

Maoni yetu yamebainisha matokeo na madhara makubwa yasiyotarajiwa na /au yasiyokusudiwa ambayo tunaona yanatokana na marekebisho yaliyopendekezwa na hasa kama marekebisho yakifanyika kwa hati ya dharula kama ambavyo serikali imependekea.

Ni imani yetu kwamba uchambuzi huu utasaidia sana kuboresha mchakato wa marekebisho yaliyopendekezwa, ili kuhakikisha marekebisho hayo yanafikia malengo yake yaliyokusudiwa kwa ufanisi zaidi na namna inayojenga. 

Hapa chini, tunawasilisha mapendekezo na maoni yetu mahsusi na ya jumla:

Sheria ya Makampuni

Tunapokea na kupongeza nia ya kuwa na uwazi zaidi kwenye vifungu na kazi za makampuni. Hata hivyo lengo tunaona kuwa lengo kuu la marekebisho haya la kutatua mkanganyiko baina ya Sheria ya Makampuni na Sheria ya NGO ni mkanganyiko wa kutengenezwa na unaoweza kutatuliwa kwa utaratibu mwingine. Ni muhimu kukumbuka kuwa mkanganyiko huu baina ya Sheria za Makampuni na NGO ulitokea baada ya marekebisho ya Sheria ya Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGOs) iliporekebishwa mwaka 2005. Pia tunaona kuwa muundo na fasili ya Makampuni yasiyo na Mtaji yanayotoa Misaada, kimsingi unapaswa kufuata viwango vya kimataifa. Mapendekezo haya ya Serikali yanaashiriwa kuwa tunachagua kwa makusudi kukwepa viwango vya kimataifa, jambo ambalo litaipelekea Tanzania kujiweka kwenye hatari isiyo ya lazima ya kupoteza imani na vivutio kwa wawekezaji. 

Hoja yetu nyingine ni kwamba, tafsiri mpya ya makampuni inayopendekezwa ni finyu, inazuia shughuli za makampuni na kuweza kuwa na athari zisizotarajiwa za kudhoofisha ubunifu na uvumbuzi. Hii ni hoja muhimu kuizingatia hasa tukiwa katika muktadha ambapo huduma na bidhaa mpya zinatengenezwa na kuzalishwa kila kukicha ambazo zinaongeza thamani kwenye maisha ya watu na uchumi wa mataifa. Ingawa mapendekezo ya Serikali yameweka kipengele cha kuruhusu shughuli nyingine za makampuni kama atakavyoridhia Waziri husika, bado tunaona kuwa kuikubali tafsiri finyu inayopendekezwa kutasababisha vizuizi badala ya kuwa kuwezesha mazingira bora ya kisiasa. 

Katika muktadha huohuo, nguvu na mamlaka aliyoongezewa Msajili kuyafutia usajili makampuni ni tatizo jingine na linaweza kusababisha wawekezaji kuwa na mashaka ya kuanzisha makampuni mapya au hatma ya makampuni yao. 

Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza

Kadri teknolojia inavyokua kila kukicha, ni muhimu kuhuisha sheria na taratibu ili ziendane na teknolojia mpya za kidijitali. Kwa dhati kabisa, tunapongeza uwepo wa vifungu vinavyolinda wafanyakazi katika sekta hii kwa kutoa sharti la kupatiwa bima wakati wanaingia mikataba ya ajira.

Ingawa marekebisho yamelenga kuongeza ajira, mapato na uwezo wa kitaalam kupitia sekta hii, tuna sababu ya kuamini kuwa marekebisho haya yakipitishwa kama yalivyo, yanaweza kuzuia kufanikisha malengo hayo. Tunaifafanua hoja hii hapa chini. 

Mosi, haturidhishwi na kuanzishwa kwa utaratibu wenye urasimu mwingi na wingi wa kodi (mzigo wa kifedha) kwa makampuni ya kigeni yenye shauku ya kutumia Tanzania kama eneo la filamu. Tunapaswa kuiona shauku hii kama fursa kwa nchi yetu na hivyo kuweka mazingira wezeshi na rahisi kwa makampuni hayo kufanikisha adhima yao wakati Taifa likijipatia faida anuwai. Faida za kiuchumi hazitokani na kutoza au kupokea fedha toka kwa makampuni hayo moja kwa moja, ambayo pia inapingana na taratibu za kimataifa, na hivyo inaweza kuwavunja moyo wateja wenye dhamira ya kuja kuwekeza nchini. Lakini faida huja kupitia kuitangaza nchi na faida za kiuchumi nyingi zinazotokana na kusaidia uendelezaji sekta ya filamu na wana-filamu kutumia fedha zao hapa hapa nchini, kama kulipa kodi, kununua bidhaa na kuajiri wafanyakazi wa hapa hapa nchini. Jambo la muhimu pia ni kutambua kuwa njia za kuvuna faida zaidi kutokana na vivutio vya asili nchini Tanzania zinahitaji muda zaidi, mapitio ya kina na tathmini pana. Aidha, kuna baadhi ya masharti hayabebeki -ambayo yanaonekana kuleta udhibiti mkubwa wa maudhui, kama vile mabango yote yanahitaji kuidhinishwa kabla ya kutumika.

Tunashauri vigezo na masharti virejee viwango vya kimataifa katika kudhibiti sekta hii muhimu inayozalisha mapato ambayo hutoa mwanga wa matumaini kwa vijana wengi. 

Sheria ya Mashirika yasiyo ya Kiserikali 

Kama waumini wa uwazi, uwajibikaji na ushirikishwaji, tunaunga mkono harakati za kuimarisha mambo haya ndani ya sekta ya asasi za kiraia. Hata hivyo, kuna mambo kadhaa tuna mashaka nayo -kwa kuzingatia tafsiri finyu ya nini maana ya mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) ambayo, ikiachwa kama ilivyo, itasababisha mashirika mengi kukosa uhalali wa kisheria. Ingawa lengo ni kutofautisha Mashirika yasiyo ya kiserikali na Asasi nyingine, tafsiri finyu ya NGOs kimsingi inayatenga na kuyafuta kabisa mashirika mengi.

Vile vile, muda mfupi uliotolewa kubadilisha usajiri ili ufuate sheria hii unaleta mashaka: kutokana na uzoefu wa siku za nyuma muda uliotolewa hautoshi kushughulikia mashirika yote ambayo yanapaswa 'kuhamia sheria mpya'. Tunapendekeza itolewe angalau miezi sita na pale inapobidi muda uongezwe zaidi. Sote tunakumbuka kuwa hivi karibuni Serikali iliongeza muda wa kusajili simu kwa njia ya mfumo wa alama za vidole ili utekelezaji wa zoezi hilo uwe na ufanisi na tija. Pendekezo la Serikali linapaswa kujifunza kutokana na uzoefu huo.

NGOs zina mchango mkubwa sana katika Taifa letu. NGOs ni chanzo cha mapato ya mamilioni ya dola ambayo karibu fedha yote hii hutumika hapa hapa nchini na huingizwa kwenye uchumi wa Taifa letu. NGOs zinaajiri maelfu ya wananchi ambao vipato hivyo vinawawezesha kumudu mahitaji muhimu ya familia na wategemezi wao. Vile vile NGOs zinalipa kodi kwa mamilioni ya shilingi na hivyo kuchangia katika bajeti ya Taifa. Na zaidi ya yote huduma zinazotolewa na NGOs zinalenga kuboresha maisha ya wananchi na kuleta maendeleo nchini. Kwa zaidi ya miongo mitatu sasa, NGOs zimechangia kwa kiasi kikubwa sana kuboresha huduma za kijamii kwenye sekta mbalimbali kama afya, maji, na elimu.  Tunaomba kamati hii itambue mchango huu muhimu sana unaofanywa na mashirika yasiyo ya kiserikali. Hivyo basi, malengo mazuri yenye nia ya kuboresha uratibu wa sekta hii lazima yahakikishe kuwa hayaathiri lengo la kuwezesha kazi zao zifanyike vizuri. Pia, ni muhimu kuhakikisha kuwa mapendekezo haya hayapelekei kubana haki za kimsingi zilizopo kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama vile uhuru wa kujieleza na kujumuika. 

Kama tungekuwa na muda wa kutosha, badala ya siku 2 tulizopata mwaliko huu, tungeweza kufanya uchambuzi wa kina kuhusu mchango wa taasisi zisizo za kiserikali katika maendeleo ya nchi yetu. Tunasistiza kuwa Serikali isifanye maamuzi kwa haraka bila kuzingatia uchambuzi yakinifu. Marekebisho yanayopendekezwa sasa yatishia uwepo wa sekta hii imara, yenye nguvu na muhimu sana. 

Sheria ya Vyama vya Kijamii 

Maoni yetu kwa kiasi kikubwa yana lengo la kuongeza uwazi kwenye vifungu kadhaa. Hata hivyo, tunatahadharisha mamlaka na nguvu alizopewa Waziri kuvifuta vyama vya kijamii, tunatoa wito mchakato wa haki uzingatiwe. 

Sheria ya Takwimu

Tumefurahi kuona marekebisho ya Sheria ya Takwimu yaliyowasilishwa yana mtazamo wa kupanua nafasi ya kukusanya, kusambaza na kutoa fursa ya mijadala kuhusu takwimu.

Kipekee tunatambua na kupongeza mapitio kadhaa yaliyopendekezwa na nyongeza ya vifungu na sura mpya ambazo:

·        Zinatoa ufafanuzi zaidi na maelezo bayana ya tafsiri mbalimbali zikiwemo zile za takwimu na tafiti

·        Zinarejesha tena kutambulika kwa takwimu zisizo rasmi au za mashirika huru ya kitakwimu kukusanya na kusambaza takwimu.

·        Zinaelezea vizuri mchakato unaopaswa kufanyika kupata maelekezo kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu

·        Zinaruhusu usambazaji wa taarifa za takwimu maalum bila kuomba ridhaa ya Serikali

·        Zinapunguza adhabu zisizo za kawaida

Hata hivyo, tunasisitiza kuwa mependekezo haya ya serikali yangezingatia maeneo mengine mawili muhimu ili kuondoa ubaguzi unaotokana na mapendekezo haya ya serikali na pia kuwezesha wadau muhimu wa ndani kuweza kuchakata na kuchapisha takwimu kwa maendeleo ya Taifa letu:

§  Mosi, kuwepo kwa utaratibu/mchakato wa wazi na huru wa kupata vibali na kufanya maamuzi yanayohusu maswala ya takwimu

§  Pili, kama ambavyo masharti ya kupata vibali yamelegezwa kwa mashirika ya kimataifa, tunapendekeza masharti pia yalegezwe kwa wadau wa takwimu wa ndani (domestic stakeholders).

Sheria ya Uwakala wa Meli

Kutokana na changamoto zilizopita, ni muhimu kuratibu na kudhibiti sekta hii kwa uangalifu na kwa umakini mkubwa. Hata hivyo, tunawasilisha kuwa mabadiliko mengi kati ya haya yana madhara hasa kwa mawakala wengi wa meli ambao hutoa huduma na ajira kwa Watanzania.

Baada ya maoni haya ya jumla, tunaambatanisha maoni mahsusi kwa kila kipengele cha Mapendekezo ya Serikali. 

Tunaomba kuwasilisha,

Centre for Strategic Litigation

Change Tanzania

JamiiForums

HakiElimu

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu

Policy Forum

Save the Children

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC)

Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA)

TIBA

Twaweza

 

 

Kwa nini tunajali? Muswada wa Marekesbisho ya Sheria Mbalimbali

Deus Valentine Rweyemamu na Anna Henga 

Jioni ya Jumatano Juni 19, 2019 asasi za kiraia kama sehemu ya wadau katika kuchangia mabadiliko ya sera na sheria mbalimbali zilipokea muswada wa marekebisho ya sheria nane tofauti ambapo mapendekezo hayo yamepelekwa kwa Kamati ya Bunge ya katiba na Sheria kwa HATI YA DHARURA. 

Mchakato wa kutunga sheria ni mgumu kwa kuwa unatumia lugha ngeni ya kiingereza na zaidi lugha ya Kisheria. Hatahivyo hakuna anayesalimika kwa sheria yeyote kwasababu ni ngumu.

Wadau tumepata muda wa chini ya masaa 48 ya kutazama na kuhitajiwa kuwasilisha maoni kwa kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria siku ya Ijumaa tarehe 21 Juni. Masaa machache yaliyotolewa hayatoshi kufikia wanachama wote na kuwasilisha maoni ya pamoja kwa bunge. Siku ya kuwasilisha maoni ilikuwa siku ya kuabudu kwa ndugu zetu waislamu na hivyo si wengi wangeweza kushiriki jambo hili muhimu. 

Kuna baadhi ya mifano ya hivi karibuni ya kufanya maamuzi yenye nia njema yaliyofanyika kwa haraka na kupelekea matokeo hasi yasiyotarajiwa. Mifano hiyo inajumuisha sheria ya Vyombo ya Habari na marekebisho ya Sheria ya Takwimu. Mabadiliko ya Sheria ya Takwimu yalipelekea wadau wa maendeleo kusitisha misaada yao kwa serikali kutokana na mapungufu yaliyopo katika sheria hiyo na kupelekea mapendekezo ya mabadiliko ya sheria kuletwa tena bungeni chini ya miezi 9 tangu mabadiliko ya mwisho kuwasilishwa bungeni. Pia tuna mifano ya hivi karibuni ya sheria kupingwa mahakamani mara tu baada ya kupitishwa (Sheria ya Vyama vya Siasa), kesi kusikilizwa na hata walalamikaji kushinda (Sheria ya Vyombo vya Habari). 

Hivyo basi, kwa kuzingatia muswada ulioletwa bungeni yaani the Written Laws (Miscellaneous Amendments Act) No. 3 (2019), tumegundua mambo walau manne yenye kutia wasi wasi: 

Athari za kiuchumi na kijamii zitakazotokana na vikwazo kwa asasi za kiraia

Endapo marekebisho haya yatapitishwa kama yalivyo, mashirika mengi ya kiraia yatafutiwa usajili na kushindwa kuanza tena. Kwa kufanya hivyo watu watapoteza ajira, watoa huduma kukosa mapato, serikali kupoteza mapato ya kodi (kodi za mapato na kodi za utendaji, pamoja na kodi zinazotokana na bidhaa na huduma zinazotumiwa na mashirika hayo).  Kulingana na ripoti ya mwaka 2018 ya shirika la Foundation for Civil Society, kiasi cha zaidi ya shillingi bilioni 11 zilitumika kusaidia mashirika nchi nzima yaliyowafikia watanzanzia zaidi ya milioni 3. Shirika hilo tangu kuanzishwa kwake limesaidia mashirika zaidi ya 5,500 Tanzania Bara na Tanzania Visiwani. Shirika la Msaada wa Kisheria LSF ambalo limesajiliwa kama NGO linatoa linatoa ruzuku kwa Wasaidizi wa Kisheria kwenye kata 2,500 nchi nzima. Wanawake wengi nchini (zaidi ya 10,000) wamenufaika na msaada uliotokana na mashirika haya kupata haki yao ya kumiliki ardhi ambapo ardhi yenye thamani shillingi ya zaidi ya billioni 2 imeokolewa mwaka jana pekee.

Marekebisho haya yataathiri watengeneza filamu wa kimataifa kwa kudhibiti matumizi ya mandhari pamoja na maudhui ya filamu nchini. Katika zama hizi ambazo wasanii wetu wanakimbilia Afrika kusini kutengeneza video na asilimia kubwa ya mapato ya bodi yanatokana na wanafilamu hao wa nje tunahitaji kuitafakari hatua hii. Muswada unapendekeza kudhibitiwa kwa matangazo kwa kuyapeleka kwenye bodi kabla ya kutolewa. Itakuwaje kwa watoa huduma, wacheza filamu, wachugaji na wengine wanaohitaji kujitangaza kama kila mmoja atahitaji kupelekea tangazo lake kwa bodi hii? 

Kwa muktadha huu, kuna hati hati ya kukiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano kwa kuvamia haki ya watu kujumuika na kufanya kazi. 

Kukosekana kwa usawa na kutokufuatwa kwa misingi ya utoaji haki na Katiba ya nchi

Asasi za kiraia kama NGOs ni mhimili muhimu sana wa amani na utangamano wetu. Wapo wasiokuwa mashabiki wa siasa ama vyama na namna pekee ya kuja pamoja ni kupitia asasi hii. Hawa watakwenda wapi iwapo msajili anapewa mamlaka ya kulalamika, kupeleleza, kuendesha mashitaka na kutoa hukumu? Msajili akiamini kampuni imejihusisha na masuala ya kijinai anaweza kuifutia usajili kampuni hiyo. Hili linaondoa haja ya kutatua mashauri haya kupitia mahakama kinyume na misingi ya haki ya kwa mujibu wa Katiba yetu ya mwaka 1977. 

Msajili mpya wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) atakuwa sasa na mamlaka ya kusimamisha asasi na kufanya uperembaji wa asasi kila baada ya miezi mitatu. Ni jambo gumu sana kutekeleza hilo kwa mashirika zaidi ya 8,000 yaliyopo nchini, na je ofisi hii ya msajili ina uwezo wa kufuatilia hili? 

Uhai wa mashirika yaliyosajiliwa chini ya Sheria ya Vyama vya Kijamii, uko chini ya matakwa ya Waziri. Waziri anapewa mamlaka ya kufuta chama cha kijamii kwa kuwa tishio kwa utawala bora wa nchi bila kuweka mipaka kwenye maana halisi ya kutisha utawala bora.  Mashirika haya hasa asasi za kidini zina wanachama mamilioni na hutoa huduma kama za afya kwa zaidi ya asilimia 40 ya watanzania. Ikitokea waziri amewafuta kwa mamlaka ya Muswada huu, watakwenda wapi wale wanaonufaika na huduma zao? 

Kunyamazisha sauti za wananchi, kupelekea taharuki na mafarakano

Watanzania tuna historia ndefu na utamaduni mzuri wa kujumuika, kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja. Marekebisho haya yanaweza kuathiri historia hii kwa kiasi kikubwa. Mashirika mengi nchini yatapata shida kufikia vigezo vipya vilivyowekwa ili kujisajili au yatashindwa kufanikisha usajili katika muda mchache uliowekwa kwa sababu zilizo nje ya uwezo wao. Urasimu pia unaweza kukatisha tamaa mashirika mapya kuanza. Kwa kiwango kikubwa hii itaathiri uwezo na utayari wa wananchi kujumuika na kutatua changamoto wanazokabiliana nazo. Tayari Sheria ya Maudhui Mtandaoni (2018) imekuwa na madhara haya kwa waandishi wa habari za mtandaoni (bloggers): blogu nyingi zilifungwa mara baada ya kutungwa kwa sheria hiyo, wengine waliomba usajili wakijua malipo ya ada yatalipwa kwa awamu na baadae wakashindwa kuendelea baada ya kutakiwa kulipa kwa mara moja. Blogu nyingi sasa zimefungwa nchini Tanzania na vijana wengi wamepoteza ajira na kipato. 

Tafsiri finyu iliyotelewa kwenye mapendekezo ya mabadiliko ya sheria mbali mbali yanaleta hatari kubwa ya kuua asasi nyingi zinazofanya kazi halali yenye umuhimu mkubwa kwa Jamii kwa kupoteza usajili na uwepo wao kisheria. Labda tusijiulize asasi hizi zitakuwa mgeni wa nani bali tujiulize watanzania wanufaika wa asasi hizi watakimbilia kwa nani?

Tuna kila sababu ya kuungana pamoja kuomba muswada huu kuondolewa bungeni ili kuruhsu muda wa kutafakari na kujadiliana.

                            

 


download REPORT Posted on : 25 June, 2019