- November 30, 2022
- Posted by: Adminct
- Category: News

Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ni kampeni ya kimataifa ya kupinga ukatili dhidi ya wanawake. Kampeni hii hufanyika kuanzia tarehe 25 Novemba na kumalizika 10 Desemba ya kila mwaka kwa ajili ya kupinga ukatili na kutetea haki za wanawake. Tarehe hii ilichaguliwa kuwaenzi akina dada wa Mirabal sisters, wanaharakati watatu wa kisiasa kutoka Jamhuri ya Dominika ambao waliuawa kikatili mwaka 1960 kwa amri ya mtawala wa nchi hiyo, Rafael Trujillo (1930 – 1961). Tarehe 20 Desemba 1993, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha Azimio la Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake kupitia azimio namba 48/104, kuweka njia kuelekea kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana duniani kote.
Hatimaye, mnamo tarehe 7 Februari 2000, Baraza Kuu lilipitisha azimio 54/134, likiitaja rasmi tarehe 25 Novemba kuwa siku ya kimataifa ya Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na kwa kufanya hivyo, kukaribisha serikali, mashirika ya kimataifa pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali, NGOs kuungana pamoja na kuandaa shughuli zilizoundwa ili kuongeza uelewa wa umma juu ya suala hilo kila mwaka katika tarehe hii ya 25 Novemba.
Lengo la kampeni hii ni kuongeza ushawishi, kubadilishana taarifa na uzoefu, kujenga uwezo wa pamoja, matumizi mazuri ya rasilimali zinazopatikana na kuunganisha nguvu za asasi za kijamii katika kuhamasisha, kuelimisha, kukemea na kuchukua hatua kwa pamoja ili kupinga ukatili wa kijinsia katika jamii.
MAMBO TUNAYOHITAJI WATANZANIA KATIKA KUADHIMISHA SIKU HIZI NI KAMA YAFUATAYO;
- Uwepo wa usawa katika upatikanaji wa elimu kwa wote watoto wa kike na wa kiume bila kuwanyanyapaa au kuwatenga kutokana na hali au jinsia zao na mambo yahusianayo na jinsia kama ujauzito. Kuwe na #ElimuBilaUbaguzi
- Kuongeza ufadhili wa muda mrefu na usaidizi kwa mashirika ya haki za wanawake yanayofanyia kazi masuluhisho madhubuti ya kuzuia na kukabiliana na unyanyasaji dhidi ya wanawake.
- Kupinga kurudi nyuma kwa haki za wanawake, paza sauti za watetezi wa haki za binadamu wanawake, na vuguvugu la wanawake wanaotetea haki za wanawake katika utofauti wao na kuhamasisha watendaji zaidi kujiunga na harakati za kukomesha unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana kote ulimwenguni iwe chachu ya kushiriki na kuunga mkono baadhi ya wanawake wanao pambania haki za wanawake kama shangazi Maria Sarungi Tsehai na shangazi Fatuma Karume.
- Kukuza uongozi na ushiriki wa wanawake na wasichana katika nafasi za kisiasa, utungaji sera, na maamuzi kutoka ngazi za kimataifa hadi za mitaa, ikiwa ni pamoja na katika michakato ya maendeleo, binadamu na amani.
- Imarisha taratibu za ulinzi ili kuzuia na kuondoa ukatili, unyanyasaji, vitisho na ubaguzi dhidi ya watetezi wa haki za binadamu wanawake na watetezi/wanaharakati wa haki za wanawake. #ChangeTanzania