Muingiliano wa Dola  na Chama Cha Mapinduzi unavyoathiri utawala nchini: 

Tanzania ni nchi  ambayo inaongozwa kwa mfumo wa utawala wa sheria, tukumbuke kwamba utawala wa sheria sio lazima uwe utawala bora au wa kidemokrasia hii ni kutokana na namna sheria zimetugwa, yaani je sheria zinatugwa kwa malengo gani? Kuna matatizo katika jamii zinataka kutatua au kuna kikundi kinataka kutumia sheria hizo kukandamiza wengine? Kwa kiasi kikubwa nchi yetu imekuwa na sheria nyingi ambazo zina malengo ya kulinda chama tawala na viongozi wake huku haki za wananchi wengine zikikanyagwa, chukulia sheria inayoweka kinga kwa DPP , Spika Wabunge  na Naibu Spika, IGP , Jaji Mkuu , Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na Rais mwenyewe kutoshitakiwa na utaratibu ambao upo kisheria katika kupata viongozi wa kuongoza awamu hadi awamu ni kupitia mfumo wa vyama vingi. Ingawa kuna mstari mwembamba sana unatenganisha CCM na watendaji wa serikali na vyombo vya dola. Hata vyombo ambavyo kwa kawaida vingetakiwa kutoa haki kwenye washindani wa kisiasa, vinaonekana kuwa na uhusiano na CCM kama vile Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, aliyewahi kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Augustino Ramadhani, alijitokeza kutaka kuwania Urais kupitia CCM. Mwaka 2020  aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha, alitangaza nia ya kutaka apitishwe na CCM kuwania urais wa Tanzania.  https://sw.wikipedia.org/wiki/Augustino_Ramadhani

Hii inadhihirisha kwamba hakuna mgawanyo wa madaraka unaofanya kazi nchini kwa sababu Katika nchi ambazo kuna mgawanyo wa madaraka na vyombo vya utoaji haki vinavyojitegemea, si rahisi kusikia Jaji Mkuu mstaafu akijiingiza kwenye uchaguzi kuomba kupitishwa na chama awe mgombea wa Urais.

Nchini Tanzania, watumishi wengi wa umma tukianza na wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya ni makada wa CCM na hata wengine wakiteuliwa kutoka vyama vingine huishia kuwa wananchama wa CCM na kutekeleza ilani ya CCM kama ilivyokuwa kwa Marehemu Anna Mghwira. Watumishi hawa wanatakiwa kuwa watumishi wa umma lakini vyeo vyao hivyo vya kiserikali vinawapa fursa ya kuingia kwenye vikao vya CCM kwa mujibu wa nyadhifa zao.  https://sw.wikipedia.org/wiki/Anna_Elisha_Mghwira

Hata matumizi ya mali za umma yamekuwa hayana vikwazo na vizuizi sana zinapokuja shughuli za CCM. Inapofika nyakati za uchaguzi, ofisi hizi za umma kimsingi hubadilika na kugeuka za CCM kwa maana ya matumizi ya rasilimali watu na nyinginezo. Kwa kifupi CCM imekuwa ikifaidikika na mfumo huu wa kufanya siasa na uchaguzi ulioizunguka kiasi kwamba watumishi wa umma wamekuwa wakiogopa kujihusisha na mambo ya vyama vya upinzani kwa kuhofia kupoteza vibarua vyao iwapo watagundulika wanaunga mkono vyama hivyo. Hii sio sawa na inaondoa uhuru kwa wananchi.

Kutokana na madaraka makubwa aliyonayo Rais yanayompelekea kukinufaisha chama chake nchini inasababisha kuathirika kwa  utawala wa sheria, upatikanaji wa haki na kuua demokrasia ambayo ndio msingi wa upatikanaji wa utawala bora. Kwa kuwa chama kimemeza mfumo wote wa utoaji haki kwa maana ya Mahakama kwa kupitia Rais ambaye ndiye anayeteua na kutengua watumishi wake muda wowote akitaka. 

Tunaamini kwamba kama wananchi wana lengo kweli la kuing’oa CCM madarakani, sehemu ya kwanza wanayotakiwa kuipigania ni kuhakikisha kunakuwa na mabadiliko ya Katiba ya Tanzania inayotumika sasa na kupata #KatibaMpya ambayo itarekebisha mfumo wa utawala na kuweka mgawanyo wa madaraka kivitendo zaidi. Afrika Kusini, Kenya, Malawi na Zambia wamefanya mabadiliko ya Katiba zao wakati wakienda kwenye chaguzi zao na matokeo yake yakawa mazuri kwa wapinzani. CCM, pamoja na mambo mengine, inaendelea kubaki madarakani kwa sababu Katiba iliyopo ilitungwa kwa lengo la kuisimika ibaki madarakani milele.

#KatibaMpya     

 #ChangeTanzania



Leave a Reply