Mapendekezo ya mabadiliko kwa mfumo wa Elimu.

Serikali imekusudia kuleta mapinduzi ya kijamii na kiuchumi ili kuibadili Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Sekta ya elimu na mafunzo, kwa mujibu wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025 na Mpango wa muda mrefu wa Maendeleo ya Taifa 2011/12 hadi 2024/25, inatarajiwa kuleta maendeleo ya rasilimaliwatu kwa kutayarisha Watanzania mahiri walioelimika na wapendao daima kujielimisha ili kuliletea Taifa maendeleo na kuliweka kwenye uchumi shindani. Ili kufikia lengo hilo, mfumo wa elimu na mafunzo unaotumika nchini lazima utoe fursa za kutosha kwa watu wengi zaidi kuelimika na kuendelea kujielimisha. Kadhalika, mfumo huu unawajibika kutoa elimu na mafunzo yenye ubora unaokubalika na kutambulika kitaifa, kikanda na kimataifa. Katika kufanikisha hili, Serikali imekuwa ikitekeleza mipango na programu mbalimbali za elimu na mafunzo. Hata hivyo, katika kipindi cha utekelezaji wa Sera cha 2015-2022, changamoto mbalimbali zimekuwa zikichangia katika kushuka kwa ubora wa elimu na mafunzo nchini. Changamoto hizo ni pamoja na udhaifu katika mfumo na muundo wa elimu na mafunzo; uhaba wa walimu; uhaba wa zana, nyenzo, vifaa na miundombinu ya kufundishia na kujifunzia; na mapungufu katika ithibati na uthibiti wa ubora wa shule na vyuo.

Toleo la Sera la mwaka 2023 linabainisha masuala ambayo Serikali, kwa kushirikiana na wadau katika elimu na mafunzo, itayawekea mkazo zaidi ili kuweka mazingira mazuri ya kufikia malengo ya

mipango ya maendeleo. Masuala haya ni pamoja na kuinua ubora wa mfumo wa elimu na mafunzo ili uwe na tija na ufanisi, kutoa fursa za elimu na mafunzo kwa usawa na kuendelea kuinua ubora wa mitaala ya elimu na mafunzo kukidhi mahitaji ya maendeleo ya Taifa. Aidha, Serikali itaendeleza matumizi ya lugha za Kiswahili, Kiingereza na Alama, pamoja na lugha nyingine za kigeni katika elimu na mafunzo. Vilevile, itaendelea kuinua ubora wa mfumo wa upimaji, tathmini na utoaji vyeti katika ngazi zote, ikiwa pamoja na utoaji wa ithibati za ujuzi katika ngazi mbalimbali. Serikali itaimarisha uwezo wa uongozi na utawala katika sekta ya elimu na mafunzo na kupanua wigo wa ugharimiaji wa elimu na mafunzo.

Dira ya elimu na mafunzo nchini ni “Kuwa na Mtanzania aliyeelimika na mwenye umahiri ikiwemo maarifa, stadi, uwezo na mtazamo chanya utakaomwezesha kuchangia katika kuleta maendeleo ya Taifa”. Vilevile, Dhima ya Sera ni “Kuinua ubora wa elimu na mafunzo kwa kuweka mifumo na taratibu zitakazowezesha kupata idadi kubwa ya Watanzania walioelimika na wanaopenda kujielimisha zaidi ili waweze kuchangia katika kufikia malengo ya maendeleo ya taifa”. Ili kufanikisha utekelezaji wa Sera hii kwa ukamilifu, kunahitajika ushiriki wa wadau wote wa elimu na mafunzo katika ngazi zote, zikiwemo sekta binafsi, Asasi za Kiraia na washirika wengine wa maendeleo.

Napenda kuwashukuru wale wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine katika mchakato mzima wa kukamilisha toleo hili la pili la Sera ya Elimu na Mafunzo.



Leave a Reply