Makala juu ya matumizi ya nishati chafu  yanavyoathiri watanzania.

Serikali kupitia wizara ya nishati inayosimamiwa na Mbunge January Yusuph Makamba imekuwa ikiwataka wananchi kutumia  nishati safi badala ya nishati chafu kwa kuwa inaathari nyingi kuanzia kiafya, mazingira na zaidi kwenye athari za mabadiliko ya tabia ya nchi. Zaidi ya asilimia 80 hutumia nishati chafu kwa matumizi ya kupika majumbani .

Kwa mujibu wa takwimu za afya zinaonyesha  watanzania 33,000 wanapoteza maisha kila mwaka kutokana na matumizi ya nishati chafu ikiwemo mkaa, kuni, mabaki ya mazao kama vile  magunzi ya mahindi na kinyesi cha wanyama takwimu hizi zinaonyesha hali ni mbaya kuliko watu wanaokufa kwa, Malaria na hata kifua kikuu. Hii inaashiria kuwa matumizi hayo yanaathiri sana Watanzania wenye kipato cha chini wasioweza kumudu gharama za nishati safi na mbadala kama majiko ya gesi na majiko ya umeme au makaa ya kutengeneza bila kutumia miti. https://jikopoint.co.tz/jiko-news/matukio/nishati-safi-ya-kupikia-kunusuru-maisha-ya-watu-33000-kila-mwaka-tanzania

Waziri wa nishati nchini mnamo Oktoba 25, 2022, alielezea kuwa athari za matumizi ya nishati chafu ya kupikia, pia alizindua  kampeni ya nishati safi ya kupikia. Katika kuangalia utekelezaji wa kampeni hakuna mabadiliko makubwa yaliyofikiwa na kampeni hiyo, lakini pia hakuna mwendelezo wa kampeni hiyo, Kikubwa kilichofanyika ilikuwa ni kongamano la mjadala  matumizi ya nishati safi ambapo Rais  Samia Suluhu Hassan aliagiza mamlaka za serikali kuunda kikosi kazi cha Taifa cha wataalamu kitakacho tengeneza mpango mkakati wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa kupikia. http://www.swahili.people.cn/n3/2022/1102/c416585-10166472.html

Baada ya hapo hakuna kingine kilichofanyika mpaka kufikia mwaka  2023, hii inaonyesha dhahiri hakuna juhudi ya  serikali kudhibiti matumizi ya nishati chafu kwa wananchi moja kwa kuweka mazingira ya kufanya nishati safi kuwa nafuu, pili kutoa elimu kwa nguvu kwa kutumia majukwaa mbalimbali .

  • Swali ni je serikali imejipanga vipi kuwezesha katika kuhakikisha Watanzania wote wanatoka kwenye matumizi ya nishati chafu kupikia? Je nishati safi ni nafuu vya kutosha kulingana na uchumi wa Watanzania walio wengi ?
  • Serikali imejipanga vipi katika kumshawishi Mtanzania ambaye anatumia nishati inayotokana na kuni anayoitafuta bure au mkaa ambao ni bei rahisi kuingia kwenye matumizi ya nishati safi ambayo atailipia na ina bei ghali?

Serikali imekuwa ikiweka mikakati  mizuri bila utekelezaji na mipango kubaki kwenye makaratasi, awali mwaka jana mwezi wa 8, Waziri January Makamba alibainisha mpango wa kuwezesha wananchi kumudu gharama za gesi na kuepukana na matumizi ya mkaa na kuni kwa utaratibu wa kumruhusu mteja kuinunua kwa bei ndogo kulingana na mahitaji yake. Alisema wananchi wengi wanashindwa kumudu kutokana na gharama kubwa zilizopo, moja ya vikwazo kwa Watanzania kutumia gesi ni kwamba lazima uwe na fedha nyingi kwa mkupuo. Wanataka kuleta teknolojia inayoruhusu mtu kununua gesi ya Sh 500 au Sh 1,000. Wataileta  sokoni ili watu waanze kununua gesi kama wanavyonunua kopo la mkaa au fungu la kuni, hivyo mchakato wa kuzipunguza unaelekea ukingoni ili kulifanyia mapinduzi suala hilo. https://bongo5.com/waziri-wa-nishati-january-makamba-amesema-serikali-kuja-na-kifurushi-cha-gesi-ya-kupikia-08-2022/

Serikali pia kupitia wizara ya afya, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu  21 Februari, 2023 aligawa mitungi midogo ya gesi kwa wajasiriamali wanawake 600 amesema kuwa matumizi ya nishati ya kuni na mkaa yamekuwa yakisababisha   saratani ya mfumo wa chakula. Ummy ameshauri kutumia nishati ya gesi kuepuka na madhara hayo. https://habarileo.co.tz/waziri-ummy-tumieni-gesi/

Kugawa mitungi ya gesi pekee haitoshi kwa kuwa hili ni jambo endelevu na pia ni matumizi ya kila siku si kwa wamama wajasiriamali tu bali watu wote majumbani na mahotelini ambapo nishati hiyo hutumika zaidi, serikali inatakiwa kuweka mifumo wezeshi ambayo kwa kiwango kikubwa itawawezesha wananchi kumudu matumizi ya gesi kwa kuwa inapatikana kwa wingi nchini, kwa nini bei iwe kubwa kiasi cha watu kushindwa kumudu?

Matumizi ya nishati chafu hasa ya kuni maeneo ya vijijini imekuwa ni changamoto sana kwa kuwa kuni zinatafutwa maporini na kupelekea watafutaji wa nishati hiyo kupoteza muda mwingi kutafuta huku shughuli zao nyingine zikilala. Pia inapelekea watoto wa kike kuwa hatarini na kutendewa vitu vibaya kama kubakwa au kupata mimba za utotoni, pia kunasababisha uharibifu mkubwa wa misitu na mazingira kwa ujumla. Serikali inatakiwa kujua hii yote inapelekea kuzorota kwa uchumi na kutengeneza Taifa tegemezi na maskini muda wote.

Sote tunaona namna mfumuko wa bei nchini Tanzania ulivyoshika kasi, Watanzania hasa wenye uchumi wa kati na chini imekuwa ni changamoto wao kumudu matumizi ya nishati safi. Wengi  wao hawamudu moja kwa moja wanatumia nishati safi pamoja na nishati chafu kwa kuwa hawawezi gharama na wengine hawawezi kabisa na kubaki kwenye matumizi ya nishati chafu.

Vitu kama hivi serikali imeonekana kutoitilia mkazo katika kushughulikia matokeo yake wanaoumia ni wananchi, kama nishati safi haina madhara kiafya serikali ingehakikisha kwa namna yoyote ile wanapunguza au kumaliza kabisa tatizo hilo

Uchumi wa Taifa letu unategemea sana watu wenye afya bora ili kusisimua uzalishaji katika nyanja zote za kiuchumi, hatuwezi kuwa na Taifa imara na kusonga mbele kama afya zetu zinazorota na magonjwa mbalimbali ikiwemo yanayotokana na matumizi ya nishati chafu ambayo yanagusa Watanzania walio wengi zaidi. Ni wakati wa serikali sasa kuonyesha kuwa wana nia ya dhati ya kuliondoa Taifa katika madhira haya na kulitoa Taifa kwenye umaskini na kuleta mbinu stahiki za kujikwamua kiuchumi, kielimu na kijamii.

#ChangeTanzaniaLeave a Reply